Zaburi 88
Kilio Kwa Ajili Ya Kuomba Msaada
Wimbo. Zaburi ya wana wa Kora. Kwa mwimbishaji. Mtindo wa mahalathi leanothi. Utenzi wa Hemani Mwezrahi.
1 Ee Bwana , Mungu uniokoaye,
nimelia mbele zako usiku na mchana.
2 Maombi yangu yafike mbele zako,
utegee kilio changu sikio lako.
3 Kwa maana nafsi yangu imejaa taabu,
na maisha yangu yanakaribia kaburi.[~1~]
4 Nimehesabiwa miongoni mwa wale waendao shimoni,
niko kama mtu asiye na nguvu.
5 Nimetengwa pamoja na wafu,
kama waliochinjwa walalao kaburini,
ambao huwakumbuki tena,
ambao wamekatiliwa mbali na uangalizi wako.
6 Umenitupa katika shimo lenye kina kirefu sana,
katika vina vya giza nene.
7 Ghadhabu yako imekuwa nzito juu yangu,
umenigharikisha kwa mawimbi yako yote.
8 Umenitenga na rafiki zangu wa karibu
na kunifanya chukizo kwao.
Nimezuiliwa, wala siwezi kutoroka;
9 nuru ya macho yangu
imefifia kwa ajili ya huzuni.
Ee Bwana , ninakuita kila siku,
ninakunyooshea wewe mikono yangu.
10 Je, wewe huwaonyesha wafu maajabu yako?
Je, wale waliokufa huinuka na kukusifu?
11 Je, upendo wako hutangazwa kaburini,
uaminifu wako katika Uharibifu?[~2~]
12 Je, maajabu yako hujulikana mahali pa giza,
au matendo yako ya haki katika nchi ya usahaulifu?
13 Lakini ninakulilia wewe, Ee Bwana , unisaidie;
asubuhi maombi yangu huja mbele zako.
14 Ee Bwana , kwa nini unanikataa
na kunificha uso wako?
15 Tangu ujana wangu nimeteseka, nikakaribia kifo;
nimepatwa na hofu zako, nami nimekata tamaa.
16 Ghadhabu yako imepita juu yangu;
hofu zako zimeniangamiza.
17 Mchana kutwa zinanizunguka kama mafuriko;
zimenimeza kabisa.
18 Umeniondolea marafiki na wapendwa wangu;
giza limekuwa ndilo rafiki yangu wa karibu kuliko wote.
<- Zaburi 87Zaburi 89 ->
*Zaburi 88:3 Kaburi hapa maana yake ni Kuzimu, kwa Kiebrania ni Sheol.
†Zaburi 88:11 Yaani Abadon.