Zaburi 30
Maombi Ya Shukrani
Utenzi wa kuweka wakfu hekalu. Zaburi ya Daudi.
1 Nitakutukuza wewe, Ee Bwana ,
kwa kuwa umeniinua kutoka vilindi,
na hukuacha adui zangu
washangilie juu yangu.
2 Ee Bwana , Mungu wangu, nilikuita unisaidie
na wewe umeniponya.
3 Ee Bwana , umenitoa Kuzimu,
umeniokoa nisishuke kwenye shimo la mauti.
4 Mwimbieni Bwana , enyi watakatifu wake;
lisifuni jina lake takatifu.
5 Kwa maana hasira yake ni ya muda mfupi,
bali upendo wake hudumu siku zote.
Inawezekana kilio kiwepo usiku kucha,
lakini asubuhi kukawa na furaha.
6 Nilipofanikiwa nilisema,
“Sitatikiswa kamwe.”
7 Ee Bwana , uliponijalia,
uliuimarisha mlima wangu,
lakini ulipouficha uso wako
nilifadhaika.
8 Kwako wewe, Ee Bwana , niliita,
kwa Bwana niliomba rehema:
9 “Kuna faida gani katika kuangamia kwangu?
Katika kushuka kwangu shimoni?
Je, mavumbi yatakusifu?
Je, yatatangaza uaminifu wako?
10 Ee Bwana , unisikie na kunihurumia,
Ee Bwana , uwe msaada wangu.”
11 Uligeuza maombolezo yangu kuwa kucheza,
ulinivua nguo za gunia ukanivika shangwe,
12 ili moyo wangu uweze kukusifu na usikae kimya.