Zaburi 143
Maombi Ya Kuokolewa Dhidi Ya Adui
Zaburi ya Daudi.
1 Ee Bwana , sikia sala yangu,
sikiliza kilio changu unihurumie;
katika uaminifu na haki yako
njoo unisaidie.
2 Usimhukumu mtumishi wako,
kwa kuwa hakuna mtu anayeishi aliye mwenye haki mbele zako.
3 Adui hunifuatilia,
hunipondaponda chini;
hunifanya niishi gizani
kama wale waliokufa zamani.
4 Kwa hiyo roho yangu inazimia ndani yangu,
moyo wangu ndani yangu unakata tamaa.
5 Nakumbuka siku za zamani;
natafakari juu ya kazi zako zote,
naangalia juu ya kazi
ambazo mikono yako imezifanya.
6 Nanyoosha mikono yangu kwako,
nafsi yangu inakuonea kiu kama ardhi kame.
7 Ee Bwana , unijibu haraka,
roho yangu inazimia.
Usinifiche uso wako,
ama sivyo nitafanana na wale washukao shimoni.
8 Asubuhi uniletee neno la upendo wako usiokoma,
kwa kuwa nimeweka tumaini langu kwako.
Nionyeshe njia nitakayoiendea,
kwa kuwa kwako nainua nafsi yangu.
9 Ee Bwana , uniokoe na adui zangu,
kwa kuwa nimejificha kwako.
10 Nifundishe kufanya mapenzi yako,
kwa maana wewe ndiwe Mungu wangu,
Roho wako mwema na aniongoze
katika nchi tambarare.
11 Ee Bwana , kwa ajili ya jina lako, hifadhi maisha yangu,
kwa haki yako nitoe katika taabu.
12 Kwa upendo wako usiokoma,
nyamazisha adui zangu;
waangamize watesi wangu wote,