64
1 Laiti ungelipasua mbingu na kushuka chini,
ili milima ingelitetemeka mbele zako!
2 Kama vile moto uteketezavyo vijiti
na kusababisha maji kuchemka,
shuka ukafanye jina lako lijulikane kwa adui zako,
na kusababisha mataifa yatetemeke mbele zako!
3 Kwa maana ulipofanya mambo ya kutisha ambayo hatukuyatazamia,
ulishuka, nayo milima ikatetemeka mbele zako.
4 Tangu nyakati za zamani hakuna yeyote aliyesikia,
hakuna sikio lililotambua,
hakuna jicho lililomwona Mungu mwingine ila wewe,
anayetenda mambo kwa ajili ya wale wamngojeao.
5 Uliwasaidia watu wale watendao yaliyo haki kwa furaha,
wale wazikumbukao njia zako.
Lakini wakati tulipoendelea kutenda dhambi kinyume na njia zako,
ulikasirika.
Tutawezaje basi kuokolewa?
6 Sisi sote tumekuwa kama mtu aliye najisi,
nayo matendo yetu yote ya uadilifu ni kama matambaa machafu;
sisi sote tunasinyaa kama jani,
na kama upepo maovu yetu hutupeperusha.
7 Hakuna yeyote anayeliitia jina lako
wala anayejitahidi kukushika,
kwa kuwa umetuficha uso wako
na kutuacha tudhoofike kwa sababu ya dhambi zetu.
8 Lakini, Ee Bwana , wewe ndiwe Baba yetu.
Sisi ni udongo, wewe ndiye mfinyanzi;
sisi sote tu kazi ya mkono wako.
9 Ee Bwana , usikasirike kupita kiasi,
usizikumbuke dhambi zetu milele.
Ee Bwana, utuangalie, twakuomba,
kwa kuwa sisi sote tu watu wako.
10 Miji yako mitakatifu imekuwa jangwa;
hata Sayuni ni jangwa, Yerusalemu ni ukiwa.
11 Hekalu letu takatifu na tukufu, mahali ambapo baba zetu walikusifu wewe,
limechomwa kwa moto,
navyo vitu vyote tulivyovithamini vimeharibika.
12 Ee Bwana , baada ya haya yote, utajizuia?