16 Wakamfanya Mungu kuwa na wivu kwa miungu yao migeni,
na kumkasirisha kwa sanamu zao
za machukizo.
17 Wakatoa dhabihu kwa pepo, ambao si Mungu:
miungu wasiyoijua,
miungu iliyojitokeza siku za karibuni,
miungu ambayo baba zenu hawakuiogopa.
18 Mkamwacha Mwamba, aliyewazaa ninyi;
mkamsahau Mungu aliyewazaa.
19Bwana akaona hili, akawakataa,
kwa sababu alikasirishwa
na wanawe na binti zake.
20 Akasema, “Nitawaficha uso wangu,
nami nione mwisho wao utakuwa nini,
kwa kuwa wao ni kizazi kilichopotoka,
watoto ambao si waaminifu.
21 Wamenifanya niwe na wivu
kwa kile ambacho si mungu,
na kunikasirisha kwa sanamu zao
zisizokuwa na thamani.
Nitawafanya wawaonee wivu wale ambao si taifa.
Nitawafanya wakasirishwe
na taifa lile lisilo na ufahamu.
22 Kwa maana moto umewashwa kwa hasira yangu,
ule uwakao hadi kwenye vina vya mauti.
Utateketeza dunia pamoja na mazao yake,
na kuwasha moto katika misingi ya milima.
23 “Nitalundika majanga juu yao
na kutumia mishale yangu dhidi yao.
24 Nitatuma njaa kali dhidi yao maradhi mabaya,
yateketezayo na tauni ya kufisha;
nitawapelekea meno makali ya wanyama mwitu,
na sumu ya nyoka wale watambaao mavumbini.
25 Barabarani upanga utawakosesha watoto;
nyumbani mwao hofu itatawala.
Vijana wao wa kiume na wa kike wataangamia,
pia watoto wachanga na wazee wenye mvi.
26 Nilisema ningewatawanya
na kufuta kumbukumbu lao
katika mwanadamu.
27 Lakini nilihofia dhihaka za adui,
adui asije akashindwa kuelewa,
na kusema, ‘Mikono yetu imeshinda;
Bwana hakufanya yote haya.’ ”
28 Wao ni taifa lisilo na akili,
hakuna busara ndani yao.
29 Laiti wangekuwa na hekima wangefahamu hili,
na kutambua mwisho wao utakuwa aje!
30 Mtu mmoja angewezaje kufukuza elfu moja,
au wawili kufukuza elfu kumi,
kama si kwamba Mwamba wao amewauza,
kama si kwamba Bwana amewaacha?
31 Kwa kuwa mwamba wao si kama Mwamba wetu,
sawasawa na vile adui zetu wanavyokiri.
32 Mzabibu wao unatoka kwenye mzabibu wa Sodoma,
na kutoka kwenye mashamba ya Gomora.
Zabibu zake zimejaa sumu,
na vishada vyake vimejaa uchungu.
33 Mvinyo wao ni sumu ya nyoka,
sumu yenye kufisha ya swila.
34 “Je, hili sikuliweka akiba
na kulifungia kwenye vyumba vyangu vya hazina?
35 Ni juu yangu kulipiza kisasi; nitalipiza.
Wakati utakapowadia, mguu wao utateleza;
siku yao ya maafa ni karibu,
na maangamizo yao yanawajia haraka.”
36Bwana atawahukumu watu wake,
na kuwahurumia watumishi wake
atakapoona nguvu zao zimekwisha
wala hakuna yeyote aliyebaki,
mtumwa au aliye huru.
37 Atasema: “Sasa iko wapi miungu yao,
mwamba walioukimbilia,
38 miungu wale waliokula mafuta ya dhabihu zao
na kunywa mvinyo wa sadaka zao za vinywaji?
Wainuke basi, wawasaidie!
Wawapeni basi ulinzi!
39 “Tazama basi, Mimi mwenyewe, Mimi Ndiye!
Hakuna mungu mwingine ila Mimi.
Mimi ninaua na Mimi ninafufua,
Mimi nimejeruhi na Mimi nitaponya,
wala hakuna awezaye kuokoa kutoka mkononi mwangu.
40 Ninainua mkono wangu kuelekea mbinguni na kusema:
Hakika kama niishivyo milele,
41 wakati ninapounoa upanga wangu unaometameta
na mkono wangu unapoushika ili kutoa hukumu,
nitalipiza kisasi juu ya adui zangu
na kuwalipiza wale wanaonichukia.
42 Nitailevya mishale yangu kwa damu,
wakati upanga wangu ukitafuna nyama:
damu ya waliochinjwa pamoja na mateka,
vichwa vya viongozi wa adui.”
43 Furahini, enyi mataifa, pamoja na watu wake,
kwa kuwa atailipiza damu ya watumishi wake,
atalipiza kisasi juu ya adui zake
na kufanya upatanisho
kwa ajili ya nchi na watu wake.
44 Mose na Yoshua[b] mwana wa Nuni wakaja, wakanena maneno yote ya wimbo watu wakiwa wanasikia. 45 Mose alipomaliza kuyasoma maneno haya yote kwa Israeli wote, 46 akawaambia, “Yawekeni moyoni maneno yote ambayo nimewatangazia kwa makini siku hii ya leo, ili kwamba mpate kuwaagiza watoto wenu wayatii kwa bidii maneno yote ya sheria hii. 47 Siyo maneno matupu tu kwenu, bali ni uzima wenu. Kwa hayo mtaishi maisha marefu katika nchi mnayovuka Yordani kuimiliki.”
Mose Aelezwa Kuhusu Kifo Chake
48 Siku hiyo hiyo Bwana akamwambia Mose, 49 “Kwea katika mapangano ya Mlima Abarimu hadi kilima cha Nebo kilichoko Moabu, ngʼambo ya Yeriko, na uitazame Kanaani, nchi ninayowapa Waisraeli kama milki yao wenyewe. 50 Utafia kwenye mlima huo unaokwea na kukusanyika pamoja na watu wako, kama ndugu yako Aroni alivyofia juu ya Mlima Hori naye akakusanyika kwa watu wake. 51 Hii ni kwa sababu ninyi wawili mlivunja uaminifu nami mbele ya Waisraeli kwenye maji ya Meriba-Kadeshi katika Jangwa la Sini, na kwa sababu hamkuuinua utakatifu wangu miongoni mwa Waisraeli. 52 Kwa hiyo, utaiona tu nchi kwa mbali; wewe hutaingia nchi ninayowapa watu wa Israeli.”
aYeshuruni maana yake ni Yeye aliye mnyofu, yaani Israeli (ona pia Kum 33:26; Isa 44:2).b Yoshua, yaani Yehoshea kwa Kiebrania, maana yake ni Yehova ni Mwokozi.